Luke 8

Mfano Wa Mpanzi

(Mathayo 13:1-9; Marko 4:1-9)

1 aBaada ya haya Isa alikwenda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye, 2 bpia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba; 3 cYoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

4 d eUmati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Isa kutoka kila mji, akawaambia mfano huu: 5“Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. 6Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu. 7Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. 8 fMbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.”

Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

9 gWanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo. 10 hNaye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “ ‘ingawa wanatazama, wasione;
ingawa wanasikiliza, wasielewe.’

11 i“Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. 12Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. 13 jZile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. 14 kZile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. 15 lLakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

Mfano Wa Taa

(Marko 4:21-25)

16 m“Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga. 17 nKwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi. 18 oKwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyang’anywa.”

Mama Yake Isa Na Ndugu Zake

(Mathayo 12:46-50; Marko 3:31-35)

19 pWakati mmoja mama yake Isa na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu. 20 qMtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”

21 rIsa akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”

Isa Atuliza Dhoruba

(Mathayo 8:23-27; Marko 4:35-41)

22 s tSiku moja Isa alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni twende mpaka ng’ambo ya ziwa.” Nao wakaondoka. 23Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.

24 uWanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!”

Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari.
25Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”

Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”

Isa Amponya Mtu Mwenye Pepo Mchafu

(Mathayo 8:28-34; Marko 5:1-20)

26 v wBasi wakafika katika nchi ya Wagerasi, ambayo iko upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya. 27Isa aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini. 28 xAlipomwona Isa, alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!” 29Wakati huo Isa alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.

30Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Legioni,”
Legioni maana yake ni Jeshi.
kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.
31 zWale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo.
Shimo hapa ina maana Abyss (shimo lisilo na mwisho), yaani Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.

32Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Isa awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu. 33 abWale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.

34Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani. 35 acNao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Isa, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Isa, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa. 36 adWale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa. 37 aeNdipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Isa aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.

38 afYule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Isa afuatane naye, lakini Isa akamuaga, akamwambia: 39“Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Isa alimtendea.

Msichana Afufuliwa, Na Mwanamke Aponywa

(Mathayo 9:18-26; Marko 5:21-43)

40 agBasi Isa aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41 ahKisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Isa, akimwomba afike nyumbani kwake, 42 aikwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.

Isa alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.
43 ajKatika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44 akHuyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Isa na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.

45 alIsa akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”

Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”

46 amLakini Isa akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”

47Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Isa. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. 48 anBasi Isa akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

49 aoIsa alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”

50Isa aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”

51 apWalipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52 aqWakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Isa akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”

53Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54 arIsa akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56 asWazazi wake wakastaajabu sana, lakini Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.
Copyright information for SwhKC